Aaron Ramsey alijiandikisha katika historia ya Arsena baada ya kuwafungia bao la ushindi katika muda wa ziada na kuwaongoza kukamilisha ushindi wa 3-2 dhidi ya Hull City na kushinda kombe la FA katika uga wa Wembley, Jumamosi.
Fainali hiyo ya kusisimua iliishia na miamba Arsenal wakifanikiwa kusitisha ukame wa miaka tisa bila kushinda kombe lolote baada ya kujitoa kwenye ahera ya kufungwa 2-0 ndani ya dakika nane za mwanzo na kukomboa magoli hao kufikia muda wa kawaida.
Huku penalti zikinukia baada ya sare ya 2-2 kulazimisha dakika 30 za ziada, Ramsey alikamilisha shambulizi la kuchangamsha lililo husisha wenzake Olivier Giroud na Tomas Rosicky na kufungulia mkwaju kutoka nje ya guu lake lililoishia kimyani.
Pata shika hiyo ilianza kwa kishindo pale James Chester alipowapatia wanyonge Hull uongozi dakika nne tu baada ya mechi kuanza pale alipopachika wavuni kutokana na sintofahamu kwenye ngome ya Arsenal iliyofanya mpira kudunda kutoka mchezaji mmoja hadi mwingine.
Vijana hao wa Steve Bruce ambao walikuwa wanashiriki fainali yao ya kwanza ya kombe la FA walijipata ndotoni pale Curtis Davies alipofunga kutoka hatua chache baada ya mpira wa kichwa kutoka mwanae meneja, Alex Bruce, ilipogonga ulingo wa lango na kumwangukia dakika nne baadaye.
Huku Arsenal, mabingwa wa kombe hilo mara kumi wakiyumbayumba, Hull nusura wawamalize na la tatu lakini beki Kieran Gibbs aliweza kuokoa kutoka kwenye laini ya goli pale Bruce alipoachiliwa huru kuunganisha kichwa chake na mkwaju wa kona.
Baada ya kupunga hewa, vijana wa Arsene Wenger walianza kutandazwa mchezo wao maarufu wa pasi fupi na walipata afueni kuu dakika ya 17 pale kiungo cha kati, Santi Cazorla, alipokomboa bao moja kufuatia mkwaju wa adhabu uliomlemea kipa Allan McGregor ingawa mlinda lango huyo alikuwa kwenye lawama.
Kipindi cha kwanza kiliisha na Arsenal wakikaba Hull koo na kuwavamia na shambulizi baada ya lingine lakini ngome yao ikibaki dhabiti.
Waliporejea kutoka kukata tama, vigogo hao wapendelewa wa kutoka London kaskazini waliimarisha kuvizia wapinzani wao lakini walikosa nafasi mara kwa mara hadi dakika 19 zilipobaki muda wa kawaida kutimia.
Mlinda ngome wa Ufaransa, Laurent Koscielny, alisawazisha kutoka hatua chache pale mpira wa kona ulipomfikia na baada ya kukosa kutoa mshindi, mechi hiyo ilienda muda wa ziada.
Arsenal waliendelea kutupa nafasi baada ya nyingine huku Hull wakionesha uchovu na kusalia ngomeni na ikisalia dakika kumi penalti zitumiwe kuwatenganisha wawili hawa, Ramsey aliibuka shujaa.
Punde si punde, mashabiki wa Arsenal Wembley na kote duniani waliwacha nyoyo kwenye midomo pale mlinda ngome kigezo, Per Metersercker na kipa wake Lukas Fabianski kufanya masiara yaliomwachilia mshambuliaji mwenye kasi, Sone Aluko, kutimuka na kufyatua mkwaju kutoka pembe ya kushoto iliyokuwa nusura itue wavuni lakini mpira ulibingirika hadi nje.
Dakika tatu baadaye, kapteni wa Arsenal, Thomas Vemaelen aliwajibika kuinua kombe na kufungulia sherehe za aina yake.
0 comments:
Post a Comment